- 46 views
Takwimu inaonyesha kwamba visa vya watoto kudhulumiwa kwa kuteswa, kuhujumiwa kwa kunyimwa haki zao, kukeketwa kwa kungolewa kwa baadhi ya viungo mwilini, kunajisiwa na hivyo kupoteza bikira kabla ya kuolewa, ukosefu wa uzazi na usalama bora, sasa imefika kileleni. Watoto hutegemea hakikisho ya usalama, hudumu, makazi, ulishaji na utunzi bora kutoka kwetu sisi wazazi na wahusika wengine. Imani ya watoto kwetu watu wazima haijawahi kutingisika kamwe, na tunapowageuka na kuwatendea kinyama na kinyume cha matarajio yao, kina wagadhabisha na kuwasononesha kweli kweli.
Kumbukeni kisa cha mtoto Wanjiku kilicho wasikitisa wote baada ya kutumwa na mamake dukani masaa ya adhuhuri hivi na kutoweka asipatikane tena. Alipopatikana baadaye katika shamba la mikahawa, ilifichuliwa na wachunguzi jinsi alivyotendewa vitendo vya kinyama. Kimya kikatanda katika kijiji chake. Uchunguzi ukafifia na mwanetu akasahaulika hivyo. Cha Mshere nacho kiliwaghadhabisha sote sisi baada ya kunajisiwa na babake mzazi katika kijiji kule Bungoma, na kikafuatiwa na kile cha mtoto Atieno aliyebakwa na mjomba wake wakati mamake alipokwenda sokoni kununua bidhaa za upishi. Na kila tunapoendelea kufungua kurasa za magazeti na kusikiza habari za mashinani redioni, matukio kama haya hayakosi kutukereketa na kupamba moto katika vinywa vya waandishi wa habari.
Lakini kisa cha hivi majuzi cha unyakuaji wa ardhi ya shule ya msingi ya Langata Road, jijini Nairobi, ilionyesha kilele cha fikra ya jamii kuhusu watoto, hasa kutoka kwa wajulikanao kuwa, "Utumishi Kwa Wote," yaani idara walinda usalama. Vitendo nilivyovitaja hapo awali kuhusu unyanyasaji wa watoto, hivi sasa vimesambaa katika udhaifu mwingine tuuonao huko Jamhuri tukufu ya Kenya: unyakuaji wa mali ya umma kiholela holela na mabwenyenye wasio aibu kamwe. Ni bayana kwamba mali ya umma hasa ya mashirika mengi ya serikali yalinyakuliwa wakati kitambo wakati wa utawala wa rais Moi. Chukua mfano wa mashirika ya serikali kama vile ya ADC, AFC, KEFFRI, KARI, na baadaye unyakuaji wa viwanja vya shule, hospitali, kumbi za kijamii, makaburi, barabara, sehemu za umma zilizotengwa kwa mapumziko au starehe, na kadharika.
Sokomoko tulioishuhudia wiki iliyopita wakati wanaharakati sugu, wazazi, walimu na watoto wa shule ya msingi ya Langata Road, ilionyesha wazi kilele cha visa vya unyakuzi wa mali ya umma katika nchi tuijivuniayo. Vurugu hilo lilinikumbusha matukio nilioyashuhudia karibu miaka 40 iliyopita, wakati wanafunzi walipokabiliana na serikali ya wadhalimu wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini, wakati askari waligeuka na kuwa hayawani kwa kuwaua wanafunzi waliokuwa wakiandamana. Shujaa Mandera angelikuwa kuwa hai wakati wa kisa cha wiki iliopita, bila shaka angegutushwa na serikali ya UhuRuto.
Kwa miaka na dahara, maovu ya kijamii kama vile visa vya ulaji na upokeaji rushwa, kashfa katika uchumi wetu na uporaji wa mali ya umma umepuuzwa na serikali zilizofuatilia. Kufunika maovu haya chini ya mkeka na kutowaadhibu wahusika, ndicho chanzo cha matukio tuliyoyashuhudia wakati watoto wasio na hatia, na waliokuwa wakidai haki yao ya kuchezea katika uwanja wao, walirushiwa vitoa machozi na walinda usalama. Pia kisa hicho kilionyesha bayana ujasiri na ujeuri mkubwa na aina ya kipekee kwa wanaojiita wawekezaji, ambao hawana majina na hulindwa ipasavyo na viongozi wakuu serikalini. Badala ya kutaja jina na majina asili ya walionyakua ardhi ya shule na kuwauzia wengine, yao yanabanwa na wanaotajwa ni wale walioinunua wakidhani kwamba cheti miliki kilikuwa halali. Huwezi kuamini kwamba, hata wakati huu ambapo Wakenya wameerefuka, kupofuka na kufahamu haki zao, mwekezaji yeyote anaweza kuonyesha ujeuri na ushabiki wake wa kunyakua ardhi ya shule kutoka jiji kuu la Kenya. Kenya haijaozeshwa na uovu huu, ila Wakenya ndio mihimili ya majanga yanayotukabili sisi.
Isitoshe! Tukumbuke kisa kingine cha makabiliano kati ya wenyeji na mnyakuzi wa shule ya Our Lady of Mercy katika mtaa wa Shauri Moyo, jijini Nairobi. Na pia tusisahau ule uvumi kwamba ardhi ya vituo vya polisi vitano huko huko Nairobi tayari vimeshanyakuliwa na wanyakuzi wajiitao wawekezaji. Idhihirike wazi kwamba, ardhi kadhaa za taasisi za serikali zimo mikononi mwa wanyakuzi ambao wengi wao waligombea viti vya utawala ili wapate ulinzi kutokana na vitendo hivyo. Diposa Mhe Mama Ngilu na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) hawadhubutu kamwe kumtaja mhusika hasua aliyewauzia wahindi wanne waliotajwa na waziri huyo. Huku Waziri wa Usalama akimtolea makataa Bi Ngilu ya masaa 24 awataje wahusika wote, nyumaye ilibainika huo ulikuwa tu sarakasi tu ya mdomo kaya, kwani hakuwataja wote. Tume ya Kitaifa Ya Adhi inawajibika kutathmini upya hati za miliki za mali yaumma popote ilipo ili wanyakuzi wakome kuzimezea mate kila wanapohitaji kugharamia maisha yao ya kifahari.
Hadi pale kutakapochipuka kiongozi atakaye ajibika na kujitolea mhanga kupambana na jinamizi hili la uporaji wa mali ya umma, watoto wetu wataendelea kunyunyuziwa mabomu ya kutoa machozi kila wanapodhubutu kudai haki zao zinginezo, kama vile kupata masomo bora, malezi bora . Visa kama hivi dhidi ya watoto wasiokuwa na hatia, ni dhihaka iliyojaa dharao, uhimili wa maovu, na ukosefu maadili kwa watawala na walinda usalamu walio tegemeo lao. Ni sharti serikali iboreshe mikakati ya pamoja, au kuunda taasi ya kushughulikia haki na maslahi ya watoto wetu, ili imani yao kwetu na kwa watawala isidorore. La sivyo, kusaga meno na kuropoka maneno ovyo ovyo hakutaleta suluhu kwa matatizo chungu nzima yanayowakabiri akina yahe.
By J. IdaVethi | jidavethi@yahoo.om