- 166 views
Olimpiki 2016 inabisha hodi huko Brazil. David Rudisha atairudisha dhahabu nyumbani. Kemboi atacheza rumba ya ushindi. Kiprop ataipeperusha bendera. Hussein Bolt atatimuka kama radi. Wakenya na Waethiopia wataonyesha ufalme wao kwenye mbio za masafa marefu. Tutajivunia ushindi wao. Tutashangilia mashindano kwenye runinga zetu. Halafu tutafanya mzaha wanariadha wengine watakapokuwa wakihojiwa kwa Kiingereza. Tutatamani waseme Kiswahili, Kikalenjin, Kiamhara au Kinyarwanda halafu matamshi yao yatafsiriwe kwa Kiingereza. Wakisema lugha zao hawatachekwa. Heshima yao itasimama kidete.
Kwa nini ninasema hivyo? Kumbuka yaliyotendeka wiki iliyopita nchini Poland. Jean Marie Myasiro, kijana Mnyarwanda mwenye umri wa miaka 19, aliivunjika rekodi ya kitaifa ya Rwanda kwenye mbio za mita 10,000. Rekodi ya awali iliwekwa mwaka 2004 na Mnyarwanda mwenzake, Valence Bihavagamuye. Jean Marie alivuma sana kwenye mitandao ya kijamii wiki jana. Lakini hakupata umaarufu kwa ushindi huu. Ushindi alioupata kwenye mashindano ya dunia ya IAAF ya vijana wenye umri chini ya miaka 20. Mashindano yaliyofanyika mjini
Bydgoszcz, nchini Poland. La hasha, Jean Marie hakupata umaarufu na kushangiliwa na kwenye mitandao kwa uhodari huu. Lakini alipata umaarufu huo eti kwa kusema Kiingereza kibaya.
Wengi wamekuwa wakimcheka kwa kusema Kiingereza vibaya. Vidio ya mahojiano yake baada ya kumaliza mbio hizo iliisambazwa kwa wingi katika WhatsApp, Facebook, Twitter, na kadhalika. "The weather in Poland cold, cold very," akasema kwa Kiingereza ambacho bila shaka kilikuwa tafsiri ya lugha yake au Kiswahili. Yaani, Poland ni baridi, baridi sana. Akasema mengine mengi. Waliosambaza vidio hiyo, hawakujali kuwa kijana huyu aliwashinda wengi ili kufuzu kushiriki mashindano ya dunia. Hawakujali aliivunja rekodi ya kitaifa ya Rwanda. Hawakujali iwapo anasema lugha zingine kama vile Kinyarwanda, Kiswahili, Kirundi, Kifaransa au lugha nyinginezo. Walijali tu kuwa alisema Kiingereza vibaya.
Imekuwa kawaida kuwacheka wanariadha wetu wanapohojiwa na wanahabari baada ya ushindi wao. Swali ambalo mimi hujiuliza ni kwa nini huwajielezi kwa lugha zao? Messi husema kihispania kwenye mahojiano yote kila mara. Na ndiye mwanasoka bora zaidi duniani. Wachina, Warusi, Waarabu, Wajapani na wengineo wanasema lugha zao na wanahabari wanatafuta wakalimani kutafsiri. Waafrika pekee ndio wanang'ang'ana kusema kiingereza na Kifaransa.
Olimpiki inaanza hivi karibuni. Wanariadha wetu Waafrika wasema Kikalenjin, Kimaasai, Ekegusii, Kinyarwanda, Luganda, Kiamhara, Kizulu, Gikuyu na lugha zingine za Kiafrika wanapohojiwa. Hakuna mtu atawacheka. Hawatajiaibisha. Watahifadhi hadhi na heshima yao. Tujivunie lugha zetu.
- Dkt. Mungai Mutonya. Dkt. Mutonya anafundisha katika Washington University in St. Louis. Soma blogu yake ya Kiswahili kwenye mmutonya.wix.com/blogu.Mutonya pia amechapisha vitabu Kiswahili.