- 71 views
Kila mjadala unapoanzishwa na viongozi na watawala kuhusu umaskini, umaskini uteketezao Wakenya, mara kimya kinafuata. Badaye lawama zinatumiwa kama silaha ya kulaumu serikali ya Hayati Kenyatta, rais mstaafu Moi, Baba Jimi na Fidel, na hivi sasa, utawala wa Rais Uhuru. Lakini kimantiki, umaskini ni nini? Kiini cha umaskini ni nini? Umaskini niliivyo ujua mimi tangu jadi, na niujuavyo hivi leo, ni hali ya Mkenya yeyote yule kutokuwa na uwezo wa kujikimu kwa kujipatia mahitaji yake muhimu kama vile chakula, maji safi, maliwato, huduma ya afya, makazi bora, elimu, mazingira safi na pia upokeaji wa habari. Kwa viongozi na watawala juzi, jana na leo, hio kwao ni lugha geni.
Tangu tujinyakulie uhuru wetu, serikali ya Kenya, mataifa ya magharibi, mashirika ya misaada kama vile Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), na pia mashirika yasio ya serikali, yamejitahidi kupunguza na kutokomeza umaskini kwa wananchi wetu, bila ufanisi. Kiasi kikubwa cha pesa kimetolewa katika miradi mbalimbali nchini lakini ngo, matokeo hayapo na hayaonekani. Tafsiri ya umaskini machweo mwa serikali na wanaoitawala ni duni na haifafanuliwi kama ilivyo. Wasioujua umaskini ni nini, kweli wanaweza kutibu nchi katika janga hili la kustaajabisha na kufedhehesha? La!
Wanavyofanya ni kupima umaskini kulingana na idadi ya watu na kipato cha taifa hisika, eti kuwa maskini ni yule aishiye chini ya dola mbili kwa siku. Kweli? Eti tena kwamba maskini wa kutupwa ni wale waishio chini ya dola moja kwa siku kama ilivyo katika nchi zinazoendelea ikiweko Kenya. Wanaoelewa umaskini ni wale wanaokerwa na kuadhiriwa na madhara yatokanayo na ukosaji wa sera nzuri za kijamii na mikakati mahususi ya kuinua hali ya Wakenya wasiobahatika kama wengine. Mashirika mengi mengi hayo hutumia fedha na wakati mwingi wakitafuta njia ya kupunguza umaskini baadala ya kuuangamiza. Na wanaopewa wajibu huo wananufaika kwa kupokea mishahara minono yakiwemo marupurupu mengine. Jiulize? Mbona umaskini ungali unaawasha na kuongezeka ingawa vita dhidi yake inapamba moto?
Umaskini kama ilivyo desturi, umekithiri nyanja zote za kijamii, hasa kwa wale waishio mashinani, mitaani kama ile ya Mathare na Kibera(Kibra), kiasi cha kwamba hata vituo vya kwenda haja ndogo na kubwa, ni hafifu na haipo. Nyuso za wanachi waishio katika sehemu hizo zimepondeka pondeka, ishara kwamba wamekata tamaa. Ahadi walizopewa na waakilishi wao, matumaini waliomiminiwa na watawala wao wakati wa kuomba kula, ni yale yale, ile ile tu. Kwa wale wasio elewa madhara ya umaskini ni nini, yasikize haya. Umaskini waweza kukuelekeza utende chochote ili angalao upate kitu cha kula. Wanaopigwa risasi kiholela holela na walinda usalama ni watoto wa maskini. Wanaowaua na kujeruhiwa wakiwatetea viongozi wao wamebaki mamlakani ni watoto wa maskini. Watoto wa vigogo hawapo karibu wakati maskini wanajitolea mhanga kuwatetea na kuwapigania baba na mama zao. Diposa umaskini upo, sio kwamba kuuangamiza ni vigumu, lakini viongozi na watawala wanaelewa kuwa, pasipo maskini, uongo wa kuwa watawatendea hili na lile, halipo tena.
Katika nchi tulimozaliwa sisi, umaskini unawakumba wakubwa na wadogo, wa kike na kiume, vijijini na mijini, waliojaa na wa mapato, na pia wale waishio katika mazingira hatarishi. Lakini umaskini ni lazima uwepo? Mizizi ya umaskini twawezaje kuingoa kati yetu? Vigezo na viwango vya umaskini vyaweza kuondolewa na serikali bila katu kutegemea misaada kutoka nje? Ni kweli yawezekana.
Lakini vizuizi vinavyosimama kati ya juhudi zote zinazotendwa kuangamiza umaskini ni tabia ya viongozi na watawala kutoonyesha moyo wa kusaidia watu wao. Maadili katika uongozi kesha meguka meguka na kuporomoka. Wananchi wanaugua kwa umaskini wa kulazimishwa. Viongozi wanatumia wakati wao sio kutumikia umma, bali kuangalia walichovuna na kupora. Misaada inayotolewa na mashirika ya misaada na wafadhili wengine zinakwishia katika akaunti za watawala. Viongozi wanatengeza utajiri wao kwa vilio vya wajane, yatima, bei ya mafuta na bidhaa muhimu zinapiga nyufa, watoto wa maskini wanaendelea kusomea nje chini ya miti kwenye vumbi kisirani, vifo vya akina mama waja wazito zaongezeka, na watoto wanafariki kutokana na magonjwa yanayoweza kutibiwa na kudhibitiwa.
Serikali ifanye nini? Tufanye nini ili kuboresha na kuimarisha hali ya maisha ya wananchi? Kutumia zile shillingi billioni sita zilizotengewa wanawake na vijana kuwapa mikopo isiyo riba. Kuhimiza uongozi bora, na kukomesha tabia na hulka ya viongozi kujilimbikiza mali.
Kuimarisha na kuzikarabati barabara, zahanati za kutosha na shule. Pengine mafunzo, uimarishaji na usimamizi kabambe wa biashara ndogo, ufugaji mifugo, uvuvi, kilimo na kadharika zaweza leta matumaini kwa hao waliojiajiri katika sekta zisizo rasmi. Kuwapa vijana wetu mafunzo ya kilimo na kuwapa vifaa na mbolea kisha kuwahimiza kutumia ujuzi waliopata kupanda mimea yenye faida katika mabonde bikira yapatikanayo sehemu nyingi kama Narok, Nyando, Kitale, Nyandarwa, na kadharika. Kuwafikilia tu wenye nguvu na walio wachache wajitajirishe katika kudhibiti uzalishaji na uuzaji kwenye soko huria ni fikra potovu. Kuwaruhusu viongozi na watawala ambao ni wasaka tonge wanaofikiria tumbo na ubinafsi wao sio suluhisho kamwe. Nafikiri tukifanya hivyo, sura za Wakenya wengi zitaanza kuona mwanga mwisho mwisho wa ngiza tondo.
By J. Idavethi | jidavethi@yahoo.com