- Add new comment
- 20 views
Jukumu la uongozi sio kitu cha kuchezewa. Kiongozi yeyote yule huhakikisha kwamba anawaongoza watu wake kwa kurahisisha jinsi wanavyoendesha mikakati yao ya kujimudu kutokana na ajira walizonazo. Ni nadra kumuona kiongozi katika nchi zilizoendelea akikiuka kanuni za kuboresha maisha ya anaowawakilisha kwa hofu kwamba hatachaguliwa tena siku sijazo uchaguzi utakapofanywa. Lakini katika Bara la Afrika, ikiwemo Kenya, uongozi ni kinyume cha matakwa na matarajio ya wapiga kura. Itakuwa vigumu katika siku sijazo kuwaenzi viongozi kama Hayati Nelson Mandera na Julius Kabarage Nyerere, ambao walijinyima katika mavazi, itifaki na kupinga ufisadi, kinyume cha marais wengi wa bara letu ambao wamekosa miongozo na miiko ya utendaji kazi.
Hivyo basi, nachukua fursa hii kuchambua uongozi wa viongozi katika taifa letu la Kenya, hasa wakati huu tunaposhambuliwa na magaidi wa Al Shabba, na pia tunapoelekea kushuhudia mkutano na maandamano yalioitishwa na chama cha upinzani cha Muungano wa Cord. Jukumu zinazopewa viongozi na wapiga kura ni mara dufu, na zinahitaji uajibikaji mkubwa, uchapakazi uliomadhubiti, na mbinu zinazolengwa kuchochea ukuaji wa uchumi, ukuzaji wa ajira na juu ya hayo, juhudi inayoweza kukuza viwanda vidogo vidogo hata vikubwa. Dhamira ya kiongozi sio kuichakachua miradi inayohamasishwa na serikali iliyo mamlakani ili isiwafaidi Wakenya wote. La!
Kiongozi wa kweli huwaasa watu wake kujiepusha na vitendo vinavyoweza kulegezalegeza gurudumu la maendeleo katika maeneo yao. Uongozi bora ni ule unaoepusha siasa za majungu, chuki, fitina, udini, ukabila na vurugu inaoweza kuhatarisha amani na maisha ya wananchi. Kiongozi bora huepusha kuingiza taifa lake katika machafuko, hasa panapokuwa na tisho la kiusalama kutoka nje. Uongozi bora haudhalilishi matumizi mabaya ya fedha za ruzuku, mafisadi, anaojifanya wanamageuzi, waporaji na wafujaji wa mali ya umma na hasua wanaonuka ukabila. Kiongozi wa kweli na wa kuheshimiwa ni hutumia shutuma na tuhuma zake kwa nia njema katika kuikosoa na kuipungia mkono wa buheri serikali iliopo.
Kiongozi wa kuaminiwa hufuata maadili yaliowekwa na sheria zilizo katika katiba kuimarisha na kuboresha maisha ya watu wake, bila kutumia wadhifa wake kujilimbikiza mali au kujinufaisha binafsi. Kiongozi mwenye hekima hatumii mamlaka yake kujiongezea posho wakati uchumi wa nchi unasuasua, mchango wa wahisani umepungua na wananchi wanahangaika kwa nyongeza ya bei mara kwa mara. Kiongozi halisi huwapa wasia adhimu watu wake kama vile madhara ya ukabila, udumushaji wa amani, na jinsi wanavyoweza kuimarisha maisha yao na jamaa zao. Kiongozi bora huwa katika mstari wa mbele kulinda maisha ya wakazi wake kwa vyoyvyote vile. Kiongozi kemkem hatuhumiwi kwa makosa ya kimaadili, udhalilishaji wa mtu au wizi, ukiwepo ubadhirifu wa mali za umma.
Na wakati poendelea kuyoyoma ili tushuhudie mkutano wa Saba Saba unaoandaliwa na Bw Raila na vigogo wenzake hapo siku ya Jumapili hii, tuyatarajie yapi baada ya yote kupangwa, kusemwa na kutendwa? Ni yapi yatakayotarajiwa kuwanufaidi wanachama wa chama cha Cord na sehemu wanazozitoka? Je, kunayo matumaini yoyote kwa wafuasi wa chama hicho ambao kwa kweli wengi wao nusra ni maskini wa kutupwa? Hali ya taifa letu kabla, wakati na baada ya maandamano hayo itakuwaje? Nani atakaye kuwa mshindi baina ya serikali, chama cha Cord, wafuasi wa chama hicho na vyombo vya kulinda usalama kwa upande mwingine? Tutarajie matokeo mema au mabaya kutokana na maandamano haya yaliyopangwa na Bw Raila?
Kwanza mama mboga hatafungua kibanda chake kwa hofu ya kushambuliwa pale ghasia zitakapozuka. Pili wakulima wa pareto, wafugaji mifugo, wavuaji samaki, hawataweza kusafirisha mazao yao kwenye soko kwa sababu wenye magari yanayosafirisha bidhaa hizo watahofia yatateketezwa. Tutashuhudia mrundiko wa maziwa yalioharibika, samaki walioozea Tatu, magari yote ya uchukuzi wa abiria yataegezwa katika machumba yanamolala. Nne, duka zote za biashara katika sehemu zote za jiji la Nairobi zitafungwa na kudhibitiwa na milango ya chuma ili yasiporwe kutokeapo ghasia. Mwisho, vigogo wa chama cha Cord watakusanyika katika migahawa ya nyota tano huku wakitazama runinga ya NTV au KTN, huku wakitabasamu kuwaona maskini hohe hahe wakipambana na walinda usalama, wakijiburudisha na vileo vya Pilsner, Tusker au Guiness, huku jamaa zao wakishangilia na kuwapongeza waandamanaji katika makao yao ya kifahari mle Karen, Muthaiga na Lavington.
Tano, wananchi wapenda amani watakomesha safari zao za kutembelea mji wetu wa Nairobi hadi siku ifuatayo ya Jumatatu. Sita, iwapo ghasia zitaripuka, wengi ya majeruhi wengi hawatakuwa watoto na jamaa za Bw Raila, Kalonzo, Muthama, Jakoyo, Orengo au Wetangula, bali watakuwa akina yahe kutoka mitaa ya Kibera, Mathare, Mukuru wa Njenga, na vijiji jirani vya Kianda, Soweto Mashariki, Gatwekera, Kisumu ndogo, Lindi, Laini Saba, Siranga, Makina na shimoni. Siku ifuatayo ya Jumatatu, Gavana wa Kaunti ya Nairobi, Bw Kidero, atatangaza hasara iliosababishwa na vurugu ya siku iliotangulia, huku akiwaomba wakazi wake waendelee na shughuli zao za kawaida. Kiasi cha kikubwa cha pesa zitakazotumiwa kufagia, kulipia fidia walioadhiriwa na kusafisha mji kingewachimbia vyoo vya kudumu, mabanda ya kudhibiti hadhi zao, maji safi iliyo salama, zahanati za kutibu magonjwa yanayoweza kutibika, barabara ipitikao na shule za vidudu na za msingi zenye hadhi na zinazovifaa vya kutosha. Swali. Uongozi upo wapi jameni?
By J. Idavethi | jidavethi@yahoo.com
Sente sana IdaVethi,
Kachelewa kusoma haya makala yako lakini unapouliza uongozi utatokapi, lazima ujue kwamba wengi wetu twajiuliza vile vile pia. Itabidi mmoja wetu ajitokeze ajitolee kuchaguliwa kuwa kiongozi. Na kwa vile naona unayaelewa maadili yanayochangia uongozi ufaao na uboreshao maisha ya wanaoongozwa, mbona usitafute nafasi kwenye uchaguzi ujao na tutakusaidia kwa hali na mali? Dr Mutua amejibanza kwenye uongozi Kaunti ya Machakos na hadi wa leo, jahazi lake lilishang'oa nanga na lasafiri vizuri sana